ZAO la tumbaku limekuwa linapigwa vita duniani na kusababisha bei yake kudorora, imeelezwa.
Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William ole Nasha alikiri kuwa zao hilo limekuwa likikabiliwa na changamoto kubwa duniani na kusababisha bei kudorora na soko lake kupungua.
“Nakiri zao hili ni zao linalokabiliwa na upinzani mkubwa sana duniani... ni zao ambalo naweza kusema ‘limeshetanishwa’ na matokeo yake bei yake imedorora sana, wanunuzi wenyewe hakuna,” alisema.
Nasha alikiri kudorora kwa bei ya tumbaku ni shida ya duniani kote. Hata hivyo, serikali inatafuta fursa ya masoko kwa ajili ya zao la tumbaku hapa nchini.
Alieleza hayo wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Serengeti, Ryoba Marwa (CCM) aliyehoji tumbaku haina soko na serikali itajenga lini kiwanda cha kuchakata tumbaku.
Katika swali la msingi, Marwa alitaka kufahamu serikali inakabiliana vipi na changamoto ya zao la tumbaku kukosa masoko, ikiwemo tumbaku ya wilaya ya Serengeti na itasaidiaje upatikanaji wa kampuni zaidi ya moja kununua tumbaku ndani ya wilaya hiyo.
Akijibu swali hilo, Nasha alisema zao la tumbaku linapigwa vita na kwamba hapa nchini wanunuzi ni wanne na kukiri kuwa hata katika nchi zingine hawana mnunuzi wa tumbaku zaidi ya wanne.
Hata hivyo, Naibu Waziri huyo alisema serikali inatafuta fursa ya masoko na kwamba hivi sasa inaangalia soko la China na fursa ya soko la shisha Misri.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni